MACHOZI YA HAKI: Ujumbe Kutoka kwa Askofu Desmond Tutu
“If you are neutral in situations of injustice, you have chosen the side of the oppressor.” – Desmond Tutu Kuna maneno ambayo hayaishi, maneno ambayo hupenya vizazi na kuvunja ukuta wa unafiki. Kauli ya Askofu Desmond Tutu, shujaa wa haki za binadamu kutoka Afrika Kusini, ni miongoni mwa maneno hayo. Ni kauli inayotufanya tusijifiche nyuma ya ukimya au uoga. Anasema, “Kama utabaki kimya mbele ya dhuluma, basi umechagua upande wa mnyanyasaji.” Ni maneno yanayochoma nafsi. Yanayoamsha dhamiri ya mtu wa kawaida, kiongozi, mwalimu, mtumishi wa umma, au raia anayetazama mateso ya wengine akiwa kimya kana kwamba hayamgusi. KUPIGA KELELE YA HAKI Leo, Tanzania na dunia nzima bado zinahitaji sauti kama ya Tutu — sauti ya ujasiri, sauti ya kweli, sauti isiyopimwa kwa hofu ya mamlaka.Watu wananyanyaswa kimfumo, vijana wanakatishwa tamaa, walalahoi wanabeba mzigo wa kodi huku wachache wakiishi kwa anasa.Wakulima wanalia bei za mazao, walimu wanalia mishahara midogo, wagonjwa wanalia dawa hospitalini, na wajasiriamali wanakata tamaa kwa vikwazo visivyoisha. Wakati haya yote yakitokea, wapo wanaosema: “Ni bora tu nyamaze, tusijiharibie maisha.”Lakini Askofu Tutu angewauliza — “Ukimya wako unamlinda nani? Aliye dhaifu au aliye na nguvu?” WAKATI UKIMYA UNAKUWA DHAMBI Kuna aina mbili za uovu: ule unaofanywa kwa mikono, na ule unaofanywa kwa ukimya.Mtu anaweza kuwa mnyanyasaji kwa kutumia maneno, mamlaka, au mfumo — lakini mtu mwingine anaweza kuwa mnyanyasaji kwa kukaa kimya anaposhuhudia dhuluma. Kiongozi anapokataa kusema ukweli kwa hofu ya kupoteza cheo, ameshiriki dhambi ya ukimya.Mwalimu anapowaona wanafunzi wakitendewa vibaya lakini akakaa kimya, amechagua upande wa mnyanyasaji.Kijana anaposhuhudia rushwa, unyonyaji, au uongo serikalini na kusema “sio kazi yangu,” basi tayari amejiunga na wale wanaoendeleza mfumo wa uovu. MFANO KUTOKA AFRIKA KUSINI Desmond Tutu hakusema haya kwa maneno matupu. Alisimama katikati ya giza la ubaguzi wa rangi — akiwa amevaa joho la kasisi, lakini akiwa na moyo wa simba.Alipaza sauti alipowaona ndugu zake weusi wakinyanyaswa, kupigwa, kunyimwa haki, na kudhalilishwa.Alihubiri upendo, lakini upendo wa kweli — ule usiosema “acha mambo yende,” bali ule unaosema “simama, sema, na tenda haki.” Tanzania, taifa lililojengwa juu ya misingi ya utu, amani, na usawa, linapaswa kuamka upya.Ukimya wetu mbele ya rushwa ni kuhalalisha rushwa.Ukimya wetu mbele ya dhuluma ni kuendeleza mateso.Ukimya wetu mbele ya uongozi wa mabavu ni kuhalalisha ukandamizaji. Kama tunataka taifa lenye heshima, lazima kila raia, kila kiongozi, kila taasisi, ijifunze kusema “hapana” pale penye uovu.Ni wakati wa kuwakumbuka manabii wa Afrika kama Julius Nyerere, Nelson Mandela, na Desmond Tutu, ambao walihubiri upendo lakini hawakuwahi kuwa vipofu wa haki. MFANO WA MAISHA YA KAWAIDA Ukiona jirani ananyimwa haki katika kijiji chako, usinyamaze. Ukiona mtoto anatendewa vibaya shuleni, usinyamaze. Ukiona wafanyakazi wanateswa, usinyamaze. Ukiona wanawake au vijana wananyanyaswa, usinyamaze.Ukimya wako ni kibali cha mateso yao. KISIMAMO CHA KIROHO Biblia inasema: “Jifunze kutenda mema; tafuteni haki, mkemeeni anayeonea, mtetee yatima, mtetee mjane.” – Isaya 1:17 Ukimya ni kinyume cha mapenzi ya Mungu.Yesu hakuishi kama mtazamaji wa maovu; alisimama, aliongea, alisulubiwa kwa sababu ya kusema ukweli.Kama kweli tunamfuata, basi hatuwezi kuwa watu wa kukaa kimya. Leo, dunia inahitaji watu wenye ujasiri wa kusema “hapana” pale penye uovu.Inahitaji viongozi wenye hofu ya Mungu, walimu wenye uadilifu, waandishi wenye ukweli, na vijana wenye maono.Usiseme, “Mimi ni mmoja tu, nitabadilisha nini?”Kumbuka, kila cheche huanza moto. Usiwe neutral. Ukikaa kimya mbele ya dhuluma, umechagua upande wa mnyanyasaji.Simama. Sema. Tenda.



